Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sekta ya kibinafsi ni muhimu katika kukabiliana na njaa: FAO

Sekta ya kibinafsi ni muhimu katika kukabiliana na njaa: FAO

Ushindi katika vita dhidi ya njaa unaweza kupatikana tu kupitia ushirikiano baina ya serikali, mashirika ya umma na mashirika ya wakulima, imesema leo benki ya ukarabati na maendeleo ya Ulaya na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO. Hayo yamesemwa katika kongamano la watunga sera katika masuala ya biashara ya bidhaa za kilimo kuhusu jinsi ya kuboresha usalama wa chakula kwa kuwekeza katika kilimo, tokea Asia ya Kati, hadi Kaskazini mwa Afrika.

Katika kongamano hilo linalofanyika Istanbul, Uturuki, benki hiyo ya Ulaya na FAO zimetoa wito kwa sekta ya kibinafsi kitaifa na kimataifa, kuwekeza kwa kiasi kikubwa na kwa njia ya uajibikaji katika kilimo, ili kutatua matatizo ya usalama wa chakula ya muda mrefu.

Mashirika hayo mawili pia yametoa wito kwa serikali kuweka mazingira ya sera zinazowezesha uwekezaji wa sekta ya kibinafsi. Akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, José Graziano da Silva amesema kuwa hakuwezi kuwepo ukombozi kutokana na njaa au usalama wa chakula bila kuhusisha sekta zote za jamii, ikiwemo sekta ya kibinafsi.