Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres na Jolie wazuru Jordan kuangazia hatma ya wakimbizi wa Syria

Guterres na Jolie wazuru Jordan kuangazia hatma ya wakimbizi wa Syria

Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, Antonio Guterres, yupo nchini Jordan hii leo ili kuangazia hatma ya wakimbizi wa Syria walioko huko. Bwana Guterres ameambatana kwenye safari hiyo na Angelina Jolie, ambaye ni balozi mwema wa UNHCR.

Shirika la UNHCR linasema zaidi ya wakimbizi 253, 000 wa Syria wameshaandikishwa katika nchi jirani au bado wanasubiri kuandikishwa. Katika Jordan, kambi ya Za’atari sasa ni makao ya wakimbizi 28,000. Shirika hilo pia limesema wakimbizi wanaelezea mashambulizi ya mizinga na ya angani ambayo yanaendelea vijijini na kwenye miji iliyoko karibu na mpaka wa Jordan.

Kuna ripoti za maelfu ya watu walolazimika kuhama makwao kusini mwa Syria, ambao wanakwenda kutoka kijiji kimoja hadi kingine, wakitafuta usalama kabla ya kuvuka mpaka. Limeongeza kuwa takriban Wasyria 10, 000 wamepiga kambi kwenye mpaka na Uturuki, wakisubiri kuandikishwa na kuruhusiwa kuingia Uturuki.