UNESCO yatoa wito kwa ulimwengu kuwazia suala la Utumwa

23 Agosti 2012

Katika kuadhimisha siku hii ya kimataifa ya kukumbuka biashara ya utumwa na kupigwa marufuku biashara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, amewasihi watu wote ulimwenguni kuwazia mabadiliko yaloletwa na biashara ya utumwa duniani, na kutoa wito kwa mataifa kuwalinda raia wao dhidi ya ubaguzi wa rangi na ajira za utumwa.

Mkuu huyo wa UNESCO, Irina Bokova, amesema misururu ya matukio ya mapinduzi yaliyotekelezwa na watumwa wakijaribu kupata uhuru wao ni mambo ya kuwazia na kuchagiza kuchukuwa hatua za kulinda haki za binadamu na kukabiliana na aina za utumwa za kisasa.

Amesema historia ya biashara ya utumwa na kutokomezwa kwa biashara hiyo, imeweka umbo la ulimwengu wa sasa, kwani imebadili ramani ya dunia, sheria, utamaduni na uhusiano wa kijamii, na hata vyakula na desturi, hasa kupitia biashara ya sukari. Adhimisho la kimataiafa la Agosti 23 ni kwa kumbukumbu ya tukio la mapinduzi lililofanyika tarehe 22 na 23 Agosti mwaka 1791, wakati watumwa katika taifa la sasa la Haiti walipoanzisha vita vya mapinduzi, ambavyo vilichangia kwa kiasi kikubwa mwanzo wa kuheshimu haki za binadamu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud