Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM watoa dola milioni 158 kwa mahitaji ya kibinadamu ambayo hayajafadhiliwa vyema mwaka 2012

UM watoa dola milioni 158 kwa mahitaji ya kibinadamu ambayo hayajafadhiliwa vyema mwaka 2012

Mkuu wa maswala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Valerie Amos, ametenga dola milioni 55 kutoka kwenye mfuko wa Mfuko wa Ufadhili wa Maswala ya Dharura (CERF), ili kuimarisha operesheni za kibinadamu katika nchi nane zenye mahitaji ya kibinadam yaliyopuuzwa.

Fedha zilizotengewa mataifa ya Afghanistan, Cameroon, Colombia, Jamhuri ya Demokrasi ya Congo (DRC), Ethiopia, Madagascar, Sri Lanka na Sudan zinafanya jumla ya fedha zilizotolewa na CERF kwa mahitaji ya dharura ambayo hayakufadhiliwa vizuri mwaka huu kufikia zaidi ya dola milioni 158. Mataifa 13 tayari yalipewa takriban dola milioni 104 katika awamu ya kwanza ya ufadhili wa dharura mwaka huu, mwezi Januari.

Bi Amos amesema, fedha za CERF hutoa ufadhili muhimu sana, na kwamba fedha hizo zitaokoa maisha kwa kuyasaidia mashirika ya kibinadamu kuwafikia watu walio na mahitaji ya dharura. Mashirika yanayotoa misaada nchini Sudan yatapokea dola milioni 14 kwa ajili ya chakula, maji na huduma za afya kuwafikia wakimbizi na jamii za wenyeji wao. Dola milioni 12 zitatolewa kwa mashirika ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, milioni kumi Ethiopia na Afghanistan kila moja.