Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dr. Asha-Rose Migiro ateuliwa kuwa Mwakilishi Maalum kuhusu HIV/AIDS barani Afrika:Ban

Dr. Asha-Rose Migiro ateuliwa kuwa Mwakilishi Maalum kuhusu HIV/AIDS barani Afrika:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amemtetua aliyekuwa naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dr. Asha-Rose Migiro kuwa mwakilishi wake maalum wa maswala ya HIV na UKIMWI barani Afrika. Dr. Migiro atairithi nafasi ya Bi Elizabeth Mataka, ambaye amepongezwa na Bwana Ban kwa kazi yake ya kufana tangu alipoteuliwa katika nafasi hiyo mwaka 2007. Dr. Migiro anatarajiwa kutumia uzoefu na ufanisi wake katika kuendeleza juhudi za kukabiliana na UKIWMI kimataifa na katika bara la Afrika, wakati alipohudumu kama naibu Katibu Mkuu tokea mwaka 2007 hadi 2012.

Katika wadhfa huo, Bi Migiro, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa UNAIDS, Michel Sidibe, walizuru baadhi ya mataifa ambayo yameathiriwa zaidi na UKIMWI, na kumfanya kuwa mchagizaji mkubwa wa usawa wa uwajibikaji kwa wanawake na wanaume barani Afrika katika kutoa huduma zinazohusiana na UKIMWI.

Pia alikuwa mstari wa mbele katika kuchagiza mikakati ya kutokomeza maambukizi ya virusi vya HIV miongoni mwa watoto wachanga ifikapo mwaka 2015, na kuunga mkono ujumbe wa Katibu Mkuu Ban Ki-Moon wa kukomesha ubaguzi na kuondoa unyanyapaa unaohusiana na HIV.

Wakati huo huo, Ban pia amemteua aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown kuwa mwakilishi wake maalum wa maswala ya elimu duniani, na Bi Leila Zerrougui wa Algeria kama mwakilishi maalum wa watoto katika maeneo yaloathiriwa na vita. Bi Zerrougui atamrithi Bi Radhika Coomeraswamy, ambaye amesifiwa na Bwana Ban kwa huduma yake ya kujitolea kwa Umoja wa Mataifa na kuendeleza na kulinda haki za watoto wanaothirika na vita.