Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano Mapya DRC Yawalazimu Watu zaidi ya 5,000 Kukimbilia Uganda

Mapigano Mapya DRC Yawalazimu Watu zaidi ya 5,000 Kukimbilia Uganda

Mapigano mapya katika kipindi cha wiki moja iliyopita kwenye jimbo la Kivu Kaskazini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, yamesababisha wakimbizi zaidi ya 5, 000 kuvuka mpaka na kuingia nchini Uganda, huku indadi isojulikana ya wengine wakihama makwao kama wakimbizi wa ndani, limesema Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani, UNHCR.

Kufikia Jumatatu wiki hii, Shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda lilikuwa limewasajili wakimbizi , 5, 075 wapya kwenye kituo cha kambi ya mpito cha Nyakabande wilayani Kisoro, ambacho kinaendelea kufurika na wakimbizi kutoka eneo la Rutshuru tangu mapigano kati ya serikali na waasi yalipopea Alhamis wiki jana, na waasi kuuteka mji wa Bunagana na Rutshuru.

Wengi wa wakimbizi wanawasili Uganda kupitia mji wa mpakani wa Bunagana, ingawa wengi wengine wanapitia maeneo mengine. Kituo cha Nyakabande, ambacho kinafadhiliwa na UNHCR na wadau wengine, tayari kina wakimbizi 11, 500, na kinabanika hata zaidi kwa kuwasili idadi kubwa ya wakimbizi wapya.