Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Atoa Wito kwa Jumuiya ya Kimataifa Kuendelea Kuisaidia Afghanistan

Ban Atoa Wito kwa Jumuiya ya Kimataifa Kuendelea Kuisaidia Afghanistan

Akizungumza katika mkutano wa kimataifa mjini Tokyo Japan Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameitolea wito jumiya ya kimataifa kuendelea kujihusisha na kuisaidia Afghanistan.

Ban amesema dunia ni lazima iendelee kushikamana na watu wa Afghanistan katika ombi lao la kuwa na usalama, utulivu na mustakhbali mwema. Amesema endapo Afghanistan itakuwa na amani basi itaweza kukidhi matakwa ya watu wake, na kutimiza matumaini ya kuwa na maisha bora kwa watu wa taifa hilo na vizazi vyao. Ban ametoa wito huo katika mkutano maalumu wa msaada wa baadaye kwa Afghanistan unaofanyika Tokyo Japan.

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

Mkutano huo unasimamiwa na mwenyeji Japan na unahudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 70 akiwemo Rais wa Afghanistan Hamid Karzai na mashirika ya kimataifa. Mkutano huo unafanyika wakati ambapo vikosi vya kigeni vikijiandaa kuondoka Afghanistan ifikapo mwaka 2014, na huu ni mkutano wa tatu wa kimataifa kwa ajili ya Afghanistan katika kipindi cha miezi mitatu.