Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa kike wapigia debe usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu Rio+20

Viongozi wa kike wapigia debe usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu Rio+20

Viongozi wa kike walioko kwenye mkutano wa Rio+20, wametia saini mchakato unaotoa mapendekezo waziwazi kuyahusisha masuala ya usawa wa kijisia na ukombozi wa wanawake katika mipango yote ya maendeleo endelevu.

Katika hafla hiyo maalum, viongozi hao wametoa wito kwa serikali zote, mashirika ya umma na sekta ya kibinafsi kufuata mfano wao na kutoa kipaumbele kwa usawa wa kijinsia na ukombozi wa wanawake katika juhudi za maendeleo endelevu. Hafla hiyo imefanyika kwenye mkutano wa viongozi wa kike kuhusu siku za baadaye wanazotaka wanawake, chini ya kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na masuala ya wanawake, UN Women, kwa ushirikiano na serikali ya Brazil.

Wamesema kupata maji na nishati safi kunaweza kuboresha maisha ya wanawake kwa kiasi kikubwa kwa kupunguza umaskini, kuwapa wanawake muda zaidi kujishughulisha na maendeleo, na kuwalinda kutokana na dhuluma na athari mbaya za mazingira. Wamesema asilimia 85 ya zaidi ya watu milioni 2 wanaofariki kutokana na athari za kupikia kwenye majiko ya kiasili yenye moshi ni wanawake na watoto.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa UN Women, Michelle Bachelet amesema, wanawake wakifurahia haki sawa na nafasi sawa, umaskini, njaa, magonjwa na hupungua, na kuchangia ukuaji wa kiuchumi. Amesema, kuendeleza usawa wa kijinsia kuna uwezo wa kujenga jamii na uchumi endelevu.