Charles Taylor akatiwa Kifungo cha Miaka 50 Jela

30 Mei 2012

Rais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor amehukumiwa kifungo cha miaka 50 baada ya kupatikana na hatia ya kusaidia na kuwezesha uhalifu wa kivita wakati wa mzozo wa wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone, ambao ulidumu mwongo mmoja.

Majaji katika mahakama maalum kuhusu Sierra Leone wamesema, kama Charles Taylor asingalitoa msaada wa kifedha na aina nyengine kwa waasi wa RUF, mzozo huo na utendaji uhalifu ungekomeshwa mapema zaidi. Majaji hao wametoa kauli kuwa, Bwana Taylor aliitumia nafasi yake kama rais kusaidia na kuwezesha uhalifu kutendeka, badala ya kuchagiza amani na maridhiano.

Wamesema pia, rais huyo wa zamani hakuonyesha kusikitishwa hata kidogo na uhalifu ulotendeka, wala hakukubali makosa ambayo kwayo amepewa hukumu.

Jaji mkuu wa hukumu hiyo, Richard Lussick kiongozi huyo wa zamani alinufaika kutokana na vito vya almasi ya Sierra Leone, ambayo alipokea kutoka kwa waasi, huku akiwapa wao silaha.

(SAUTI YA RICHARD LUSSICK)

Jopo la majaji kwa kauli moja linakuhukumu kifungo cha miaka 50 kwa makosa yote ambayo umepatikana na hatia. Bwana Taylor hajakubali kuwajibika makosa haya. Jopo la majaji linatambua kuwa, kama rais wa Liberia, Bwana Taylor alishikilia nafasi muhimu ya umma, na yenye mamlaka makuu, ambayo aliyatumia vibaya kwa kusaidia na kuwezesha utendaji wa makosa ambayo amehukumiwa. Bwana Taylor aliitumia nafasi yake ya kipekee, ikiwemo uwezo wake kutumia rasilmali na vyombo vingine vya serikali kusaidia na kuwezesha utendaji uhalifu wa kivita Sierra Leone, badala ya kutumia mamlaka yake kuchagiza amani na utulivu katika eneo zima.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter