Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP na BigTime wachangisha fedha kupambana na njaa

WFP na BigTime wachangisha fedha kupambana na njaa

 

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP limeichagua kampuni ya masoko ya simu za mkononi ya BigTime ili kutekeleza mpango wa kampeni ya kuchangisha fedha kutumia ujumbe mfupi wa simu hizo wakilenga maeneo ya Mashariki ya Kati, Afrika na Ulaya.

Kampuni ya BigTime inatoa huduma kama maswali ya ujumbe mfupi kwa waendashaji wa simu za mkononi, na wateja ambao wanashiriki kujibu maswali hayo wanaingizwa katika bahati nasimu ili kushinda zawadi mbalimbali.

Kupitia kampeni hizi ambazo kila moja itadmu kwa miezi mitatu BigTime itaisaidia WFP kukusanya kiasi kikubwa cha fedha. Wanaoshiriki kujibu maswali hayo pia watapata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu WFP na njia nyingine za kujihusisha katika vita dhidi ya njaa.

Uhusiano biana ya wadau hao wawili unatumia faida ya ushirikiano kati ya waendeshaji wa simu za mkononi na wateja, ili kuruhusu WFP kuingia zaidi katika uwanja wa kuchangisha fedha kupitia simu za mkononi.