Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awataka waasi wa Mali kusitisha vita na kutafuta suluhu ya amani

Ban awataka waasi wa Mali kusitisha vita na kutafuta suluhu ya amani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameungana na Baraza la Usalama katika kuwataka waasi wa Tuareg nchini Mali ambao wanaendesha mashambulizi, uporaji na kushikilia baadhi ya maeneo Kaskazini mwa nchi hiyo kukomesha mapigano yote na kutafuta suluhu kwa njia ya amani kupitia mazungumzo ya kisiasa.

Katika taarifa yake iliyotolewa Alhamisi kupitia msemaji wake Ban amelielezea tamko la Baraza la Usalama kuwa ni lenye uzito na la wazi na linapaswa kutekelezwa bila kuchelewa.

Katibu Mkuu amerejea kuahidi msaada katika juhudi za kikanda ili kupata suluhu ya amani na  ya muda mrefu kwa mgogoro wa Mali kwa lengo la kumaliza uaasi na kurejesha utawala na hadhi ya taifa hilo.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limesema limelazimika kufunga ofisi zake nchini Mali baada ya kuporwa na pia imeahamisha baadhi ya wafanyakazi wake. Msemaji wa WFP ni Elizabeth Byrs.

(SAUTI YA ELIZABETH BYRS)