Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni muhimu kuwasaidia wajasiriamali wa mashinani kuhamia uchumi unaojali mazingira:UNEP

Ni muhimu kuwasaidia wajasiriamali wa mashinani kuhamia uchumi unaojali mazingira:UNEP

Shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP limesema kuwasaidia wajasiriamali wanamazingira wadogowadogo kunaweza kusaidia kukabiliana na changamoto za nishati, kilimo na usalama wa chakula na pia kusaidia kuhamia katika uchumi unaojali mazingira.

Huu ni ujumbe uliotolewa kwenye kongamano lijulikanalo kama SEED mjini Pretoria Afrika ya Kusini Alhamisi, kongamano ambalo linasherehekea mafanikio ya mashinani katika upande wa kijamii na biashara zinazohusiana na mazingira Afrika na maeneo mengine.

Washiriki kwenye kongamano hilo ni pamoja na washindi wa tuzo la SEED, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, serikali, sekta za biashara, jumuiya za kijamii na wanazuoni.

UNEP imesema dunia hivi sasa inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa, usalama wa chakula, ukosefu wa ajira kwa vijana na umasikini, lakini inazo fursa nyingi ambazo ni fikra bora, kujizatiti, mtazamo na ujasiri na vyote vikitumika matatizo mengi yatatatuliwa.