Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini yaahidi kuwa na jeshi la serikali lisilohusisha watoto

Sudan Kusini yaahidi kuwa na jeshi la serikali lisilohusisha watoto

Kundi la Sudanese People’s Liberation Army (SPLA) la Sudan Kusini leo limetia saini makubaliano na Umoja wa Mataifa yaitwayo “mpango wa hatua” wakirejea nia yao ya kuwaachilia watoto wote katika jeshi lao. Mpango huu mpya wa hatua umesainia na wizara ya ulinzi, mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini UNMISS, UNICEF na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watoto na migogoro ya silaha Radhika Coomaraswamy.

Mpango huo pia unahakikisha kwamba wanamgambo wote ambao wanajumuishwa kwenye SPLA hawahusishi watoto. Tangu mwaka 2005 SPLA imeorodheshwa katika kundi la orodha ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa la makundi yanayowafunza na kuwatumia watoto jeshini. Ingawa mpango huu mpya ni msisitizo wa ahadi iliyowekwa mwaka 2009 , SPLA  kama jeshi la taifa linatia saini mpango huo kwa mara ya kwanza. Bi Coomaraswamy amesema hii ni siku muhimu kwa watu wa Sudan Kusini, sio tuu unahakikisha kwamba jeshi la taifa SPLA halitohusisha watoto, bali makundi yote yaliyokubali msamaha wa serikali lazima yawaachie watoto wote. Na amesema ili makubaliano hayo yawe na maana yoyote ni lazima yatekelezwe.

Naye mwakilishi wa UNICEF nchini humo Dr Yasmin Ali Haque ameunga mkono kauli ya Coomaraswamy. Utiaji saini hii leo unafuatia hatua kama hiyo mwaka 2011 kati ya Umoja wa Mataifa na jeshi la serikali la Afghanistan, Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati.