Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asifu makubaliano ya kisiasa nchini Somalia

Ban asifu makubaliano ya kisiasa nchini Somalia

Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema ameridhishwa na makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa katika mkutano wa kikatiba nchini Somalia. Amesema kwamba ni hatua muhimu katika jitihada za kumaliza kipindi cha serikali ya sasa ya mpito na kuleta mfumo mpya wa kikatiba.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake,  Ban amesema wadau walioshiriki katika mkutano huo uliomalizika Ijumaa mjini Garowe wanastahili pongezi kwa jitihada na kuwajibika kwao.

Viongozi wa taasisi za mpito nchini Somalia, wabunge, wawakilishi wa majimbo, pamoja na mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu nchini Somalia Augustine Mahiga walihudhuria mkutano huo, ambao umefanyika wiki moja kabla ya kongamano la kimataifa kuhusu Somalia litakalofanyika mjini London baadaye wiki hii.

Taasisi za serikali ya mpito ya Somalia ziko katika mchakato wa kutekeleza mpango utakaopelekea kuundwa kwa mfumo mpya wa utawala utakao chukua nafasi ya utawala baada ya kipindi cha sasa  kumalizika  hapo Agosti.