Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNODC kutoa mafunzo ya kupambana na ufisadi kwa mashirika ya kijamii ya Afrika

UNODC kutoa mafunzo ya kupambana na ufisadi kwa mashirika ya kijamii ya Afrika

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na madawa na uhalifu UNODC imesema wakati matukio ya hivi karibuni kwenye ulimwengu wa Kiarabu yameonyesha kuwa ufisadi unaweza kukandamiza taasisi za kidekomrasia, kudumaza uchumi na maendeleo na kuchangia kutokuwepo usalama, jumuiya za kijamii zinaweza kuwa na jukumu muhimu katika kupambana na ufisadi.

UNODC inasema jumuiya hizo hazitokuwa tu kama wachunguzi wa serikali bali pia msaada kwa serikali katika kutoa huduma kwa raia kwa njia ya uwazi na demokrasia.

Ili kuziwezesha jumuiya za kijamii za Afrika kuchangia katika utekelezaji wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na ufisadi na mchakato wa kutathimini utekelezaji wa mkataba huo UNODC kwa msaada wa shirika la maendeleo la Australia inaandaa mafunzo kuanzia Machi 20 hadi 23 mwaka huu mjini Johanesburg Afrika ya Kusini .

Katika siku nne za mafunzo washiriki watajifunza masuala muhimu ya mkataba huo, watafundishwa jinsi ya kushirikiana na serikali, vyombo vya habari na sekta binafsi kusaidia utekelezaji wa mkataba katika ngazi ya jamii, taifa, kanda na kimataifa.