Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM na Luxembourg washirikiana kuimarisha huduma za simu za dharura

UM na Luxembourg washirikiana kuimarisha huduma za simu za dharura

Muungano wa kimataifa wa mawasiliano wa Umoja wa Mataifa IT na serikali ya Luxembourg wametangaza kwamba wameafikiana kushirikiana ili kuimarisha mawasiliano ya dharura na huduma za haraka pale kunapozuka majanga ya asili. ITU na Luxenberg wote ni wajumbe wa kitengo cha dharura cha mawasiliano ECT ambacho kinaundwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa misaada ya kibinadamu.

Serikali ya Luxembourg imeanzisha mfumo wa mawasiliano wa satellite uitwao “emergency.lu kwa lengo la kusaidia mashirika ya misaada ya kibinadamu kutoa msaada kwa jamii zilizoathirika na majanga ya asili, vita au matatizo mengine makubwa. Mfumo huo pia unaweza kutumika kwa muda mrefu katika maeneo ambayo majanga ya kibinadamu yanajirudia au kama sehemu ya mikakati ya maandalizi kwenye nchi zinazoendelea.

Mfumo huo wa pamoja utakuwa tayari kutumika na jumuiya ya misaada ya kimataifa kuanzia Januari mosi 2012, ambapo serikali ya Luxemborg imetoa Euro milioni 17 kufadhili uanzishwaji wake, utekelezaji wake, operesheni zake na kuufanyia ukarabati.