Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay aonya juu ya ghasia za baada ya uchaguzi nchini DRC

Pillay aonya juu ya ghasia za baada ya uchaguzi nchini DRC

Kamishina Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay Alhamisi amelaani mauaji na vitendo vingine vya ghasia vilivyotekelezwa na majeshi ya usalama ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na wafuasi wa vyama vya siasa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge katika siku chache zilizopita.

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini humo imekuwa ikifuatialia ghasia zinazoambatana na uchaguzi katika nchi nzima na inachunguza ripoti kwamba zaidi ya watu 10 wanadaiwa kuuawa na majeshi ya usalama na wafuasi wa vyama vya siasa, huku wengine wengi wakijeruhiwa mjini Kinshasa tangu tarehe 26 Novemba.

Pillay amesema viongozi wa vyama vyote vya siasa wana jukumu muhimu katika wakati huu wa kihistoria DRC na ni wajibu wao kumaliza mivutano iliyopo kwa njia ya amani na watambue kwamba wanaweza kuwajibishwa kwa vitendo vyao na pia matendo yanayotekelezwa na wafuasi wao.

Bi Pillay pia amesisitiza wajibu wa serikali ya Congo chini ya sheria za nchi hiyo na za kimataifa kuhakikisha inalinda haki za binadamu za watu wake hasa za kuishi na kuwa na usalama. Amewataka pande zote kujizuia kuendeleaza ghasia na kutafuta suluhu kwa njia ya amani.