Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango mpya wa kupambana na Ukimwi utaokoa maisha ya mamilioni ya watu

Mpango mpya wa kupambana na Ukimwi utaokoa maisha ya mamilioni ya watu

Zaidi ya watu milioni saba maisha yao yanaweza kuokolewa katika muongo ujao kwa kuwekeza katika njia mpya za kuzuia maambukizi mapya ya HIV. Hayo yamesemwa na naibu mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na ukimwi UNAIDS PaUl De Lay siku ya Alhamisi ambapo dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya ukimwi inayosherehekewa kila mwaka Desemba mosi.

Bwana De Lay amesisitiza haja ya kupunguza kwa nusu maambukizi ya HIV kwa njia ya ngono na kujidunga sindano za mihadarati na pia kuhakikisha kwamba hakuna mtoto yeyote anazaliwa na virusi vya HIV. Ameongeza kuwa katika mpango huo mpya wa uwekezaji , nchi lazima zisaidiwe ili kuhakikisha kwamba mipango yake ya HIV na ukimwi inaendelea.

(SAUTI YA PAUL DE LAY)

Tunakadiria kwa kutumia mpango huu mpya takribani maambukizi mapya kwa watu milioni 12.2 yanaweza kuepukwa kati ya mwaka 2011 na 2020 na vifo milioni 7.4 vinavyohusiana na ukimwi vitazuiliwa katika kipindi hicho. Lakini ili kufanikisha matokeo haya juhudi za mapambano lazima zifadhiliwe kikamilifu.