Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika inaonyesha matumaini katika ukuaji wa uchumi:Migiro

Afrika inaonyesha matumaini katika ukuaji wa uchumi:Migiro

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi. Asha Rose Migiro amesema bara la Afrika linatia matumaini katika ukuaji wake wa uchumi. Akizungumza mjini Addis Ababa Ethiopia kwenye mkutano wa muungano wa Afrika na shirika la mpango wa maendeleo kwa Afrika NEPAD Bi Migiro amesema mkutano huo unafanyika katika wakati ambao una changamoto nyingi na matumaini makubwa.

Amesema baraza la Afrika linakabiliana na vitisho vingi na wakati huohuo Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wanaimarisha ushirikiano ili waweze kufikia azima ya kulisaidia bara hilo. Ameongeza kuwa licha ya changamoto Afrika inaonyesha matumaini makubwa katika ukuaji wa uchumi, kwani kwa wastani uchumi wake umekuwa kwa asilimia 5.5 katika miaka ya karibuni na bara hilo ni maskani ya mataifa 6 kati ya kumi ambayo uchumi wake unakuwa kwa kasi duniani. Amesema nchi za Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara ni moja ya maeneo ambayo yameonyesha kutotikiswa sana na matatizo ya uchumi yanayoikabili dunia hivi sasa. Bi Migiro amekaribisha pia mkakati wa miaka 10 ambao ni mpango wa kuujenga uwezo kwa muungano wa Afrika.