Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita na ongezeko la majanga ni kikwazo cha suluhu ya wakimbizi:Guterres

Vita na ongezeko la majanga ni kikwazo cha suluhu ya wakimbizi:Guterres

Kuongezeka kwa migogoro na vita na kukumbwa na majanga ya asili kunafanya kuwa vigumu kupata suluhisho la watu milioni 43 duniani ambao ni wakimbizi, wakimbizi wa ndani na wale wasio na utaifa limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Kwa mujibu wa mkuu wa shirika hilo Antonio Guterres, juhudi kubwa za jumuiya ya kimataifa zinahitajika kuzuia vita, kupata suluhisho la mabadiliko ya hali ya hewa na njia bora za kudhibiti majanga ya asili. Akizungumza mjini Geneva bwana Guterres ameonya juu ya hatari ya kuongezeka kwa chuki dhidi ya raia wa kigeni kwamba ni tishio kubwa la ulinzi dhidi ya wakimbizi.

Amesema ukubwa wa tatizo la wakimbizi katika mwaka uliopita umekuwa changamoto kwa jumuiya ya kimataifa hasa katika jukumu lake la kuwalinda wale wanaotafuta hifadhi na usalama nje ya mipaka yao.