Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID na wahisani wengine wahitimisha ziara ya wiki moja Jebel Mara

UNAMID na wahisani wengine wahitimisha ziara ya wiki moja Jebel Mara

Mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kwenye jimbo la Darfur Sudan UNAMID na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa na ya kimataifa ikiwemo OCHA, UNICEF, UNHCR, WHO na baraza la wakimbizi la Denmark DRC wamehitimisha operesheni maalumu ya wiki moja kwenye eneo la Magharibi la Jebel Marra. Eneo hilo lilikuwa limetengwa kwa miaka miwili sasa kutokana na vita.

Operesheni hiyo iliyoanza Agosti 7 hadi 14 imetathimini mahitaji ya jamii za eneo hilo na kuwapelekea msaada wa kibinadamu watu katika vijiji vya Golo, Killin, Sarong, Golol, Thur na Nertiti. Kwa mjibu wa UNAMID timu hiyo ilishindwa kufikia jamii za Kurtum na Kiwilla kama ilivyopanga kutokana na vikwazo vya kisalama. Operesheni hiyo imethibitisha kwamba watu wapatao 400,000 wamesambaratishwa na vita Jebel Mara na wamepata msaada kidogo sana katika miaka michache iliyopita na kwa sasa wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.