Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano la tatu la kimataifa kuhusu dawa za kulevya nchini Kenya

Kongamano la tatu la kimataifa kuhusu dawa za kulevya nchini Kenya

Wasomi wa kiislamu barani Afrika pamoja na wenzao kutoka bara Asia wamekamilisha mkutano wa siku nne mjini Mombasa, Kenya, kuzungumzia njia muafaka za kukabili utumiaji wa dawa za kulevya.Baadhi ya maafikiano katika mkutano huo ni kushirikisha jamii nzima katika kutatua tatizo la dawa za kulevya, hasa kwa kufuata maadili ya kidini.

Kongamano hilo lilishirikisha wajumbe kutoka mataifa 16 ya Afrika na Asia wanachama wa COLOMBO PLAN, ambao ni mpango wa kusaidia wananchi katika mataifa hayo kushughulikia tatizo la mihadarati.Umoja wa Mataifa kupitia  ofisi ya Umoja wa Mataifa  inayohusika na madawa ya kulevya na uhalifu UNODC pia uliwakilishwa katika kongamano hilo lililofadhiliwa na serikali ya Marekani.

Wajibu wa Colombo Plan iliyobuniwa mwaka wa 1951 ni kulainisha njia za kupunguza kiu ya utumiaji wa dawa hizo. Njia moja iliyozungumziwa huko Mombasa ni kuhakikisha waathiriwa wa mihadarati wanakubalika na jamii hata baada ya kujirekebisha, na ufuatiliaji halisi kwa kuwapa ajira au kuwarudisha masomoni.

Mombasa ilipendekezwa kuandaa kongamano hilo kutokana na idadi kubwa ya watu wanaotumia mihadarati katika pwani ya Kenya.Wajibu wa misikiti na dini kwa jumla ulijadiliwa, katika vita dhidi ya dawa za kulevya.Wasomi wa kiislamu walifanya vikao vyao, kulikuwa na vikao vya makundi ya kijamii, na pia vijana walifanya vikao pembeni kujadili wanayofahamu kuhusu uraibu huo. Waathiriwa wa sasa na wale waliojinasua pia walipata fursa ya kuzungungumza, na hata kukutana na wataalamu wa masuala ya akili.

Kongamao hilo pia lilifadhiiliwa na Supreme Counncil of Kenya Muslims, National Campaign Against Drug Abuse Authority (NACADA) in Kenya, na pia Beareau for International Narcotics & Law Enforcement Affairs (I.N.L).Nchi zilizowakilisha katika kongamano la Mombasa ni: India, Indonesia, Sri Lanka, Pakistan, Philipines, Malaysia, Uganda, Kenya, Ghana, Albania, DR Congo, na Marekani.

Zifuatazo ni sauti za washiriki waliozungumza na mwandishi wa habari Josephat Kioko aliye mjini Mombasa, Kenya.