Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkurugenzi mkuu wa IMF ajiuzulu

Mkurugenzi mkuu wa IMF ajiuzulu

Mkurugenzi mkuu wa shirika la fedha duniani IMF Dominique Strauss Khan amejiuzulu. Bwana Strauss-Khan anayekabiliwa na mashitaka ya ubakaji dhidi ya mfanyakazi wa hoteli mjini New York hapa Marekani ameiarifu bodi ya wakurugenzi ya IMF kwamba ameamua kujiuzulu mara moja.

Amesema amechukua uamuzi huo ili kulinda hadhi ya taasisi hiyo ya kimataifa aliyoitumikia kwa heshima na taadhima, kwa nguvu na moyo wote. Pia amesisitiza kwamba anataka kutumia ari, nguvu zake zote na muda wake kuuthibitishia ulimwengu kuwa hana hatia.

Makao makuu ya IMF yapo Washington D.C na shirika hilo linajukumu la kuangalia maendeleo ya masuala ya fedha,ili kusaidia kuhakikisha hali ni shwali, pia inawajibika na kuzikopesha nchi zinazokabiliwa na matatizo ya kifedha. Mjadala unaoendelea hivi sasa ni nani atakayerithi wadhifa huo ambao umekuwa kwa miaka mingi ukishikiliwa na mtu kutoka bara Ulaya na hasa hasa Ufaransa.