Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajali ya ndege yauwa wafanyakazi wanne wa UNODC

Ajali ya ndege yauwa wafanyakazi wanne wa UNODC

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon na mkuu wa ofisi ya Umoja wa mataifa inayohusika na madawa na uhalifu UNODC wameelezea kushitushwa na huzuni yao kufuatia vifo vya wafanyakazi wane wa UNODC na marubani wawili wa kijeshi waliouawa kwenye ajali ya ndege nchini Bolivia walipikuwa wakielekea kufuatilia uzalishaji wa coca.

Wakuu hao wa Umoja wa Mataifa wametuma salamu rambirambi kwa ndugu, jamaa, marafiki na familia za wafanyakazi hao na marubani wa kijeshi wa Bolivia.

Ban amesema kupoteza kwao maisha katika kupambana na uzalishaji wa mihadarati ni changamoto waliotuachia sote. Watu wote sita waliokuwa kwenye ndege hiyo walikufa ilipoanguka Kaskazini Mashariki mwa mji mkuu La Paz mwishoni mwa wiki.

Mkurugenzi mkuu wa UNOCD Yuri Fedotov amesema ofisi yake hufuatilia kila wakati uzalishaji wa mihadarati katika sehemu mbalimbali duniani ili kutayarisha ripoti ya dunia kuhusu mihadarati.

Amewataja wafanyakazi waliokufa katika ajali kuwa ni Leonardo Ivan Alfaro Santiago, Patricia Delgado Rua, Mariela Cithia Moreno Torreblanco na Stephan Javier Compos Ruiz.