Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM watiwa hofu na mauaji ya watu 14 Abyei

UM watiwa hofu na mauaji ya watu 14 Abyei

Wanajeshi wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan wamepata miili ya watu 14 katika eneo la Abyei watu ambao huenda waliuawa kwenye mapigano mapya katika eneo hilo linalozozaniwa kati kati mwa Sudan.

Wanajeshi hao walitumwa katika eneo la Todach ambapo awali kuliripotiwa mapigano ambapo miili hiyo ilipatikana. Msemaji wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kouider Zerrouk amesema kuwa hata hivyo walinda usalama hao hawakuweza kubaini aliyehusika kwenye mauaji hayo.

Kumekuwa na hali ya wasiwasi katika eneo la Abyei kwa miezi sasa wakati eneo hilo likiendelea kuzozaniwa kati ya Sudan Kaskazini na Kusini eneo ambalo litajitenga kirasmi kutoka sehemu zingine za Sudan mwezi Julai mwaka huu.