Waasi wa FDLR wafikishwa mahakamani Ujerumani

4 Mei 2011

Kesi ya viongozi wawili wa Kihutu kutoka Rwanda wanaoshutumiwa kuandaa mauji Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeanza mjini Stuttgart Ujerumani.

Ignace Murwandashyaka mkuu wa FDLR na makamu wake Straton Musoni wote wanaishi Ujerumani. Viongozi hao wanakabiliwa na makosa 26 ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na 39 ya uhalifu wa kivita.

Viongozi hao wanashutumiwa kwa kuagiza wanamgambo kufanya mauaji ya halaiki na ubakaji kati ya Januari 2008 hadi Novemba 2009 walipokamatwa. Mshutumiwa wa tatu Callixte Mbarushimana aliyekuwa anaishi Ufaransa amepelekwa kukabili mashitaka kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC.

Umoja wa Mataifa umepongeza kesi hiyo na kusema ni hatua muhimu hasa baada ya wito uliotolewa mara kadhaa na baraza la usalama la kutaka viongozi wa FDLR wanaoishi nje kufikishwa kwenye mkono wa sheria. Murwanashyka mwenye miaka 47 ameishi Ujerumani kwa miaka 20 na Musoni mwenye miaka 49 ameishi Ujerumani tangu mwaka 1994 na amekuwa makamu wa FDLR tangu 2004.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter