Skip to main content

Kyrgystan imetakiwa kutimiza mapendekezo ya ripoti:Pillay

Kyrgystan imetakiwa kutimiza mapendekezo ya ripoti:Pillay

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay amekaribisha ripoti iliyotolewa leo na tume ya uchunguzi ya Kyrgystan na kuitaka serikali ya nchi hiyo kuchukua hatua za haraka kutekeleza mapendekezo ya ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inataka uchunguzi zaidi ufanyike na hatua za kisheri zichukuliwe kufuatia machafuko ya kikabila yaliyokatili maisha ya watu 470 mwezi Juni 2010 na kuwafanya maelfu kuwa wakimbizi wa ndani na nje. Pillay amesema ripoti hiyo itasaidia juhudi za Kyrgystan kukabiliana na ukwepaji wa sheria na kushughulikia masuala ya uwajibikaji.

Ameongeza kuwa hakutaweza kuwa na maridhiano bila kutendeka haki na amesema anaamini ripoti hiyo itafungua njia ya kuweza kuyafikiwa yote.

Pillay amesema ripoti hiyo inasema mbali ya watu 470 waliokufa wengine 1900 walijeruhiwa, zaidi ya 400,000 kuachwa bila makazi , idadi ya wanawake isiyojulikana walibakwa na uharibifu mkubwa na makazi na miundombinu ulifanyika.