Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo ya polio inamalizika leo Sudan Kusini:UNICEF

Chanjo ya polio inamalizika leo Sudan Kusini:UNICEF

Kampeni kubwa ya chanjo ya polio imeanza Sudan Kusini ikiwalenga watoto wa chini ya miaka mitano katika eneo hilo lililoshuhudia mlipuko uliosababisha vifo vingi mwaka 2008 baada ya kuwa bila polio kwa miaka mingi.

Kampeni hiyo inafanyika kwa msaada mkubwa wa Umoja wa Mataifa, na visa zaidi ya 60 vya maambukizi ya ugonjwa huo vilithibitishwa na kuwaweka watoto katika hatari kubwa kwani wengi hawakuwa wamepata chanjo.

Mkurugenzi wa UNICEF wa mpango wa kampenzi Sudan Kusini Yasmin Haque amesema chanjo hiyo ya siku tatu iliyoanzia mjini Juba inamalizika leo, lakini amesema kuna haja ya kuelimisha umma kuanzia mashinani ili waelewe umuhimu wa kuhakikisha watoto wanapata chanjo zote za polio.

Hii ni awamu ya pili kufanyika Sudan Kusini tangu mwanzo wa mwaka huu. Licha ya changamoto watoto zaidi ya 3000 wamepata chanjo katika miaka mitatu iliyopita, imesema UNICEF. Kampeni hiyo imefanyika kwa ushirikiano na serikali ya Sudan Kusini, UNICEF, shirika la afya duniani WHO na shirika la Marekani kwa ajili ya maendeleo ya kimataifa USAID.