Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wiki tatu baada ya tetemeko bado msaada unahitajika Japan:UM

Wiki tatu baada ya tetemeko bado msaada unahitajika Japan:UM

Wiki tatu baada ya tetemeko la ardhi na tsunami nchini Japan Umoja wa Mataifa unasema bado kuna mahitaji makubwa ya kibinadamu ambayo hayajafanikishwa. Umoja wa Mataifa unasema bado taratibu na matatizo ya kiufundi yanasumbua.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibindamu OCHA inasema changamoto kubwa kwa sasa nchini Japan ni hali mbaya ya usafi kwenye vituo vinavyohifadhi watu 250,000 waliohamishwa. Kwa mujibu wa OCHA kuna ongezeko la matatizo ya kuhara ambayo ni ushahidi kwamba hali ya usafi inazidi kuzorota katika vituo hivyo.

Pia upungufu wa mafuta bado ni suala linalosumbua na kuzuia wanaojitolea na mashirika ya misaada kuwafikiwa waathirika. Zaidi ya watu 10,000 wamethibitishwa kufariki dunia na wengine 18,000 hawajulikani waliko kufuatia tetemeko la Machi 11 idadi hiyo inajumuisha pia watoto 1000.

Na baada ya OCHa kufanya utafiti kwenye vituo hivyo imegundua pia waathirika wengi wanahitaji msaada wa afya ya akili, wamearifiwa pia kupatwa na muwasho, huzuni na matatizo ya kutolala.