Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya waandamanaji yanaiweka syria pabaya:Pillay

Mauaji ya waandamanaji yanaiweka syria pabaya:Pillay

Amani na Usalama

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay mwishoni mwa wiki ametoa wito wa kujifunza kutokana na matukio yanayoendelea Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.

Amesema matukio hayo yanaonyesha bayana kwamba kutumia nguvu na ghasia dhidi ya wanaoandamana kwa amani sio tuu kwamba haitatui matatizo ya wanaoandamana mitaani bali pia inaiweka nchi hiyo katika hatari ya kughubikwa na hasira, ghasia, mauaji na mtafaruku mkubwa.

Bi Pillay amesema tangu mwanzoni mwa mwaka huu dunia imeshuhudia matukio mengi ambapo serikali katika nchi mbalimbali zimetumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji, na kuongeza kuwa hakuna popote ambako njia hiyo imefanikiwa, bali imechochea jazba na hamasa mpaka kufikia hali mbaya.

Pillay amesema na hali ikishafurutu ada inakuwa ni vigumu sana kufanya maamuzi ambayo yangefanyika mapema kama kuwahakikishia waandamanaji haki yao ya kujieleza kwa amani na uhuru, kusikilizwa na kujaribu kutatua masuala ambayo yanawakera kama ukosefu wa haki za binadamu.