Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kura ya maoni ifanyike kwa haki na uhuru Sudan:Mkapa

Kura ya maoni ifanyike kwa haki na uhuru Sudan:Mkapa

Mkuu wa jopo la Umoja wa Mataifa linalofuatilia mwenendo wa upigaji kura ya maoni Sudan Kusin Bwana Benjamin Mkapa ametaka pande zote zinazohusika kwenye uchaguzi huo kujiepusha na vitendo ambavyo vinaweza kutia dosari uchaguzi wenyewe.

Wananchi hao wa Sudan Kusin watapiga kura January 9 mwakani kuamua kama wajiundie dola jipya ama eneo hilo liendelea kubaki kwenye himaya ya Sudan.

Bwana Mkapa ambaye ni rais wa zamani wa Tanzania amesema kuwa zoezi la upigaji kura ni hatua muhimu kwa wananchi wa eneo hilo lakini hatua ya utoaji matokeo ya uchaguzi huo ni suala linalotiliwa macho zaidi kwani ndilo litalobainisha nama mwenendo wa uchaguzi huo ulivyofanyika.

Mkapa ambaye alikuwa akizungumza Mjini Juba na Makamu wa rais wa Sudan Kusin Riek Machar amezitolea mwito pande zote kuhakikisha kwamba kura hiyo ya maoni inafanyika katika mazingira ya haki na uwazi. Ameitaka pia Khartoum na Juba kuhakikisha kwamba maafisa watakaosimamia uchaguzi huo wanalipwa posho zao kwa wakati ili kuepusha hali ya manung'uniko na kuharibu upigaji kura wenyewe.