Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahakama za UM zimeomba msaada wa fedha kwa baraza kuu la UM

Mahakama za UM zimeomba msaada wa fedha kwa baraza kuu la UM

Wakuu wa mahakama za Umoja wa Mataifa za uhalifu ambazo zinawahukumu wanaodaiwa kutekeleza mauaji Yugoslavia ya zamani na Rwanda zimesema zinapiga hatua katika kukamilisha kazi zake.

Wakuu hao wakizungumza kwenye baraza kuu la Umoja wa Mataifa hii leo wamesema lakini shughuli zao zinakwamishwa na upungufu wa fedha na kuondoka kwa baadhi ya wafanyakazi wao wenye uzoefu.

Jaji Dennis Byron raia wa mahakama ya kimataifa ya mauaji ya Rwanda ICTR ameliambia baraza la Umoja wa Mataifa wakati akiwasilisha ripoti yake kwamba pamoja na juhudi zetu zote tunakabiliwa na kikwazo kikubwa ambacho ni sauala la wafanyakazi, tunaendelea kupoteza wafanyakazi wazuri wenye uzoefu wanakwenda kwenye mashirika mengine ambako wanaweza kupata mkataba wa muda mrefu, akitaja kwamba wafanyakazi 167 wameondoka ICTR kati ya Julai 2009 na Juni 2010.

Jaji Byron amesisitiza kwamba wafanyakazi ni kiungo kikubwa kwa kukamilisha kazi za mahakama hiyo iliyoanzishwa Novemba 1994 kuwahukumbu waliofanya na kuchagiza mauaji ya kimbari nchini Rwanda ambako Watutsi laki nane na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa kwa mapanga katika siku 100.

Amesema licha ya changamoto zote hizo mahakama hiyo iliyopo Arusha Tanzania imepiga hatua kubwa katika kukamilisha kesi zinazotakiwa kumalizika kabla ya misho wa 2011.

Naye Rais wa mahakama ya kimataifa ya kuhukumu kesi za Yugoslavia ya zamani ICTY jaji Patrick Robinson amesema tatizo hilo la wafanyakazi pia limeathiri paubwa shughuli za mahakama hiyo, ameongeza kuwa pamoja na kwamba mahakama imeongeza idadi ya kesi inazoshughulikia kwa kipindi maalumu kutoka sita hadi 10 lakini hakuna ongezeko la fedha.

Jaji Robinson amesema ingawa wanakabiliwa na matatizo ya fedha na wafanyakazi wamepata mafanikio kadhaa katika kukamilisha kesi za mahakama hiyo iliyoko mjini The Hague Uholanzi. Mahakama ya ICTY ilianzishwa ili kuwahukumu wanaodaiwa kufanya mauaji wakati wa vita vya Balkan miaka ya 1990 na ameliomba bara kuu la Umoja wa Mataifa kuzisaidia mahakama hizo kukamilisha kazi zake.