Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAIDS yakaribisha ahadi ya wahisani kwa Global Fund

UNAIDS yakaribisha ahadi ya wahisani kwa Global Fund

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya ukimwi UNAIDS limekaribisha hatua ya wahisani kuahidi kutoa dola bilioni 18 kusaidia mfuko wa kimataifa yaani Global Fund kupambana na ukimwi, kifua kikuu na malaria.

Ahadi hizo zimetolewa mjini New York jana kwenye mkutano maalumu wa kuchagiza wahisani kuchangia zaidi kwa mfuko huo. Na hakikisho la dola bilioni 11.7 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia 2011 hadi 2013 limetolewa.

Fedha hizo zitatoa uwezo zaidi kwa Global Fund kuzisaidia nchi mbalimbali zinazojitahidi kufikia malengo ya maendeleo ya milenia hapo 2015 hasa yanayohusiana na afya. Huo ndio mchango mkubwa kabisa kuwahi kutolewa kwa Global Funda na Marekani pekee itatoa dola bilioni 4 ikiwa ni ongezeko la asilimia 38 ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita.

Nchi zaidi ya 40 zikiwemo zinazoinukia kiuchumi, mashirika binafsi na mashirika ya uuma wameahidi kuhakikisha fedha hizo zinapatikana na kusaidia kupambana na maradhi hayo matatu yanayouwa mamilioni ya watu kila mwaka.