AMISOM, IGAD na UNPOS, wameitaka serikali ya mpito ya Somalia kufanya kazi pamoja kwa ajili ya amani:

AMISOM, IGAD na UNPOS, wameitaka serikali ya mpito ya Somalia kufanya kazi pamoja kwa ajili ya amani:

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Somalia Dr Augustine P. Mahiga, mwakilishi maalumu wa mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika kwa ajili ya Somalia balozi Boubacar Diarra na mpatanishi wa IGAD kwa ajili ya amani na maridhiano ya kitaifa Somalia mheshimiwa Kipruto Arap Kirwa, katika taarifa yao ya pamoja wamesema mgawanyiko wa hivi sasa kati ya uongozi wa serikali ya mpito na shirikisho la taasisi za mpito TFI\'S nchini Somalia hausaidii na unazidi kuvuruga mipango ya amani.

Taarifa hiyo imetolewa baada ya wajumbe hao watatu kuzuru Mogadishi Septemba 9 na kufanya majadiliano na Rais Sheikh Sharif Ahmed, na wametoa wito wa TFI'S kuwa wastahimilivu na kujali maslahi ya taifa na amani.

Mahiga, Diarra na Kirwa wamesema kipindi cha mpito kitamalizika Agosti 2011 na hivyo kuifanya serikali iliyopo kuwa na muda wa chini ya mwaka mmoja kukamilisha majukumu muhimu yaliyosalia.

Na wamerejea wito wao wa umoja wa kitaifa kama hatua ya lazima kwa ajili ya kufikia amani na usalama Somalia na kuwaondolea adha mamilioni ya wananchi. Wamesema wanaofaidika na mgawanyiko huu ni wale wenye itikadi kali wanaopigana kuchukua udhibiti wan chi.