Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sheria zinazo nyanyapaa wenye ukoma zifutwe:UM

Sheria zinazo nyanyapaa wenye ukoma zifutwe:UM

Wataalamu binafsia wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametaka sheria zote zinazowabagua watu wenye ukoma zifutwe.

Wataalamu hao wanasema ingawa ukoma umetokomezwa katika nchi nyingi katika tatizo kubwa la afya ya jamii lakini bado unaambatanishwa na unyanyapaa wa hali ya juu. Kamati ya ushauri ya baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa iliyo na wataalamu 18, imeandaa kanuni na muongozo pia mapendekezo kwa nchi kufuta sheria za kibaguzi ili kuhakikisha kwamba watu wanaoumwa ukoma hawabaguliwi katika ajira, afya, ndoa na matumizi ya maeneo ya umma.

Ukoma ni ugonjwa wa muda mrefu sana katika historia ya mwanadamu, unatibika endapo utabainika mapema na ulemavu unaosababishwa na ugonjwa huo unaweza kukingwa. Hata hivyo kihistoria watu wenye ukoma na familia zao wamekuwa wakidharauliwa na kutengwa. Shigeki Sakamoto mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo anasema hadi pale unyanyapaa dhidi ya ugonjwa huo utakapoondolewa , basi jumuiya ya kimataifa itaweza kusema imetokomeza ukoma.

Watu wenye ukoma na familia zao kwa miaka mingi wamekuwa wakitengwa na serikali na jamii ambazo zinaamini ukoma unaweza kuambukiza na wanahofia ulemavu unaosababishwa na ugonjwa huo.

Shirika la afya duniani WHO linakadiria kwamba katika robo karne zaidi ya watu milioni 15 wenye ukoma ambao huathiri jamii zilizo masikini watakuwa wametibiwa na kupona. Lakini licha ya hatua hiyo nzuri maelfu ya watu bado wanaugua ukoma katika maeneo mbalimbali nab ado wanakabiliana na unyanyapaa.