Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID yaingilia kati baada ya risasi kufyatuliwa kambi ya Kalma Darfur

UNAMID yaingilia kati baada ya risasi kufyatuliwa kambi ya Kalma Darfur

Vikosi vya kulinda amani Darfur vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika UNAMID vimeingilia kati moja ya kambi kubwa kabisa duniani ya wakimbizi wa ndani baada ya hofu kutanda kufuatia kufyatuliwa kwa risasi.

Kwa mujibu wa UNAMID mvutano ulizuka jumamosi usiku kuhusu hali ya sasa ya mchakato wa amani na watu wenye silaha wakaanza kufyatua risasi usiku huo kwenye kambi ya Kalma Kusini mwa Darfur, kambi ambayo inahifadhi wakimbizi wa ndani laki moja. Watu hao wenye silaha wamejitambulisha kama wafuasi wa kundi lililomeguka la Abdul Wahid la Sudan Liberation Army SLA, ambalo ni moja ya makundi ya waasi yanayopambana na serikali ya Sudan tangu 2003.

UNAMID inasema mvutano umekuwa ukishika kasi Kalma tangu duru ya karibuni ya mazungumzo ya amani kati ya serikali na waasi kumalizika wiki iliyopita mjini Doha Qatar, huku baadi ya wakimbizi wa ndani kambini hapo wakidai kutowakilishwa ipasavyo. Hakuna aliyekufa katika sakata hiyo bali mtu mmoja amejeruhiwa kwa risasi na washukiwa wawili wamekamatwa. Pia masheikh watano wameomba hifadhi kwenye majengo ya UNAMID.