Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM umelaani shambulio dhidi ya kituo cha Al-Arabiya nchini Iraq

UM umelaani shambulio dhidi ya kituo cha Al-Arabiya nchini Iraq

Maafisa wawili wa Umoja wa Mataifa wamelaani shambulio dhidi ya kituo cha televisheni cha Al-Arabiya mjini Baghdad leo asubuhi.

Mshambuliaji wa kujitoa muhanga amearifiwa kuendesha basi hadi kwenye kituo hicho na kuuwa watu sita na kujeruhi wengine 20. Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq Ad Melkert amesema waandishi wa habari nchini Iraq wameanza tena kuwa walenga wa mashambulio ya kigaidi. Amezitolea wito pande zote nchini humo kushirikiana pamoja katika kuchukua hatua dhidi ya mashambulio hayo yanayowauwa waandishi wa habari.

Naye mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni Irina Bokova ameongeza sauti yake katika kulaani shambulio hilo akisema waandishi wa habari ni lazima waweze kuwa huru kutimiza wajibu wao bila kuhofia maisha yao. Ameitaka serikali ya Iraq kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha waliotekeleza shambulio hilo wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria.