Skip to main content

Mahakama ya UM imeamuru kesi ya wapiganaji wa zamani wa Kosovo ianze tena

Mahakama ya UM imeamuru kesi ya wapiganaji wa zamani wa Kosovo ianze tena

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa ajili ya Yugoslavia ya zamani ICTY mjini The Hague leo imeamuru kukamatwa na kufunguliwa tena kesi waziri mkuu wa zamani wa Kosovo Ramush Haradinaj kwa uhalifu wa vita.

Uamuzi huo wa kitengo cha rufaa cha mahakama hiyo umetolewa miaka miwili baada ya Haradinaj na washutumiwa wengine wawili kufutiwa mashitaka yote 37 ya uhalifu dhidi ya Waserbia wakati wa vita vya Kosovo mwaka 1998 hadi 1999. Mahakama imesema Haradinaj atashitakiwa tena kwa makosa sita ikiwemo mauaji,ukatili na unyama dhidi ya wafungwa, makosa yanayodaiwa kufnywa na jeshi la ukombozi la Kosovo KLA ambalo lilikuwa kundi la wapiganaji wa msituni wa kabila la albania.

Makamanda wenzake Haradinaj wa jeshi hilo la KLA Idriz Balaj na Lahi Brahimaj pia wanashitakiwa tena.

Tangu ilipoanzishwa miaka 17 iliyopita mahakama hiyo imeshawatia hatiani watu 161 kwa uhalifu wa vita uliofanyika Yugoslavia ya zamani. 129 kesi zao zimekamilika na wengine 33 zinasikilizwa sasa.