ILO imeonya juu ya tishio jipya la mtikisiko wa uchumi na ukosefu wa ajira
Ongezeko la kuyumba kwa masoko ya fedha na matatizo ya madeni barani Ulaya huenda yakauweka uchumi wa dunia na jitihada ya kujikomboa katika ajira kwenye hatari tena.
Taarifa hii ni kwa mujibu wa ripoti ya ofisi ya mkurugenzi mkuu wa shirika la kazi duniani ILO Juan Somavia itakayojadiliwa wiki hii kwenye mkutano wa ILO. Bwana Somavia anasema juhudi za kimataifa zimeweka malengo ya kazi bora katika mipango ya kutengamaa kwa uchumi. Lakini kuna hofu kwamba hatua za kufikia malengo hayo huenda zikawa katika hatari kutokana na hatari mpya iliyojitokeza kwenye mtikisiko wa masuala ya fedha.
Katika ripoti hiyo "kutengamaa na kukua pamoja na kazi za maana" Bwana Somavia anaonya kwamba licha ya kuwepo na dalili za kuanza kutengamaa kwa uchumi , hatari ya hatua nyingine ya matatizo ya kifedha kutokana na madeni imejitokeza , na kutishia matarajio ya kukua kwa uchumi wa baadhi ya nchi na hiyo kuathiri uchumi wa kimataifa na kutia mashaka ya kurejea kwa hali ya kawaida ya mfumo wa fedha duniani.
Pia ripoti hiyo inasema ingawa hali ya uchumi imeanza kutengamaa lakini tatizo la ajira linaendelea kuongezeka katika nchi nyingi mwaka huu wa 2010.