Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kusitishwa matumizi ya watoto vitani

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kusitishwa matumizi ya watoto vitani

Maafisa wawili wa Umoja wa Mataifa leo wametoa wito wa kuachwa mara moja vitendo vya kuwafunza na kuwaingiza watoto jeshini nchini Somalia.

Maafisa hao wanasema vitendo hivyo vimeongezeka na vinatoa athari kubwa watoto ambao wengine ni wadogo sana wa umri wa miaka tisa. Radhika Coomaraswamy ambaye ni mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya watoto na migogoro pamoja na Anthony Lake mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, katika taarifa yao ya pamoja wamesema wameshitushwa na kusikitishwa kubaini kwamba mafunzo ya kivita na kuingiza watoto jeshini yanayofanywa na makundi yenye silaha yanaongezeka nchini Somalia.

Wamesema kutumiwa kwa watoto na majeshi na makundi ya wapiganaji ni makosa ya uhalifu wa kivita, na ni lazima vitendo hivyo viachwe mara moja. Wamezitaka pande zote kuwaachilia huru watoto walionao kwa sasa na kuhakikisha wanaofanya vitendo hivyo wanafikishwa kwenye mkono wa sheria.