Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa azuru nchi za Ghuba

Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa azuru nchi za Ghuba

Kamishina Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay amezungumzia juhudi zinazopigwa kuimarisha haki za binadamu katika nchi za Ghuba.

Bi Pillay ameyasema hayo akizilenga nchi sita zinazounda baraza la ushirikiano la nchi za Ghuba, lakini pia alielezea hofu yake juu ya mambo kama haki za wanawake, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kukusanyika na uhuru wa kuwa na vikundi.

Mambo mengine aliyoyagusia ni haki za kiuchumi na kijamii, haki za watoto na matatizo ya usafirishaji haramu wa watu, ambapo amesema hatua kiasi zimepigwa. Ameyasema hayo alipohutubia katika chuo kikuu cha mfalme Abdullah kilichopo Jeddah Saudi Arabia ambako ni kituo cha kwanza cha ziara yake katika mataifa sita ya Ghuba.

Katika hotuba yake amesema kuwa elimu ikiwa ni pamoja na vyuo vikuu hivi sasa inapatikana zaidi kwa wanawake katika eneo hilo, amesema kuwekeza katika elimu hususani kwa wanawake sio tuu kwamba ni haki bali ni sera muhimu kwa maendeleo ya jamii.