Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban amewataka Wakyrgystan kumaliza mzozo kwa amani na kufuata katiba

Ban amewataka Wakyrgystan kumaliza mzozo kwa amani na kufuata katiba

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo ametoa wito tena kwa pande zinazokinzana nchini Kyrgyzstan kurejesha amani na utulivu.

Ban amewataka watumie katiba na njia ya amani kumaliza mzozo ulioshuhudia watu wakiuawa na Rais kupinduliwa baada ya maandamano yaliyoambatana na ghasia wiki jana. Na maandamano hayo bado yanaendelea. Katika taarifa iliyosomwa na msemaji wake Ban amesema anafuatilia kwa karibu na akiwa na hofu juu ya kuendelea kukiuka katiba nchini Kyrgystan na vitisho vya kutumia nguvu.

Machafuko hayo yaliyosababisha vifo vya watu wengi katika nchi hiyo ya Asia ya kati na yalisababisha kuundwa kwa serikali ya mpito na kiongozi wa upinzani mjini Bishkek, wakati Rais Kurmanbek Bakiyev alipokimbilia kusini mwa nchi hiyo.

Uongozi huo wa mpito umearifiwa kuondoa kinga ya Rais Bakiyev na umesema utamkamata endapo atakataa kujisalimisha. Naye kiongozi huyo aliyepinduliwa amesema atajiuzulu tuu endapo atahakikishiwa usalama wake na wa familia yake