Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Balozi mwema wa UHNCR ataka wakimbizi wa ndani Bosnia wasaidiwe

Balozi mwema wa UHNCR ataka wakimbizi wa ndani Bosnia wasaidiwe

Mwigizaji maarufu na balozi mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi Angelina Jolie yuko Bosnia Herzegovina kutembelea wakimbizi wa ndani.

Wakimbizi hao ni mamilioni ya watu waliolazimika kuzihama nyumba zao wakati wa vita vya miaka ya 1990, na bi Jolie ametoa wito wa kuwepo suluhisho la mateso yanayowakabili wakimbizi hao.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na UNHCR zaidi ya watu milioni 2.2 walilazimika kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na vita hivyo vya mwaka 1992 hadi 1995.

Jolie aliwasili nchini humo jana akiambatana na mzazi mwenzie Brad Pitt ili kutanabaisha adha wanayoipata Wabosnia 113,000 na wakimbizi wengine 7,000 kutoka Croatia ambao wengi wao wanaishi katika vituo vya wakimbizi.