Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-moon ametoa wito wa juhudi za pamoja kupambana na uhalifu.

24 Februari 2010

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa wito wa kuwepo na juhudi za pamoja ili kupambana na uhalifu. Akizungumza kwenye mjadala wa baraza la usalama kuhusu vitisho vya kimataifa dhidi ya amani na usalama , amekumbusha jinsi nchi wanachama walivyoungana kukabiliana na magonjwa, umasikini, mabadiliko ya hali ya hewa na ugaidi.

Amezitaka nchi wanachama kushikamana tena katika kukabiliana na uhalifu wa kimataifa ,na akisistiza kuwa tayari kuna baadhi ya hatua zimeshaanza kuchukuliwa.

Hatua hizo ni pamoja na juhudi za baraza kupiga vita dawa za kulevya, mchakato wa Kimberly wa kupinga almasi zitokanazo na umwagaji damu, na mpango wa kimataifa wa UM kukomesha usafirishaji haramu wa watu.

Pamoja na juhudi hizo bwana Ban amesema bado kuna mengi yanaweza kufanyika kukabiliana na vitisho vya kimataifa vinavyoibuka, kama uhalifu wa kutumia mtandao, usambazaji fedha haramu, uhalifu wa kimazingira na umwagaji wa taka za sumu.

Bwana Ban pia amezikumbusha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutofumbia macho masuala ya haki na utawal wa sheria na kwamba haki za binadamu daima ziwekwe mbele katika juhudi za kudhibiti uhalifu.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter