Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon ametangaza kwenye mkutano na waandishi habari Ijumatatu kwamba Wangari Maathai, mzalendo wa Kenya, aliotunukiwa Tunzo ya Amani ya Nobel na mtetezi wa mapinduzi ya kijani ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Amani wa UM mpya, atakayeshughulikia majukumu ya kuhifadhi mazingira na udhibiti bora wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani. KM aliwaambia wanahabari wa Makao Makuu, Profesa Maathai atatambulishwa rasmi kama Mjumbe wa Amani Ijumanne alasiri, kwenye taadhima maalumu itakaofanyika Copenhagen, ambapo Mkutano wa UM kuzingatia itifaki mpya ya kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa bado unaendelea na majadiliano yake. KM alisema uteuzi wa Profesa Maathai ulikuwa ni wa bora kabisa, kwa sababu ya mafanikio kadha aliopata kwenye bidii za muda mrefu za kutunza mazingira, na katika kuimarisha maendeleo. Profesa Wangari Maathai ni mwanamke wa KiAfrika pekee aliyetunukiwa Tunzo ya Nobel, na ameshatumikia Serikali ya Kenya kama waziri, na vile vile aliwahi kuwa mbunge, ni mwanataaluma na mtetezi shupavu wa haki za wanawake kwa zaidi ya miaka arobaini.

Navi Pillay, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu ametangaza mwito maalumu unayoyasihi yale mataifa ambayo bado yanaendelea kutoa adhabu ya kifo, kuzuia rasmi hukumu hii, kwa matumaini, hatimaye, wataifuta kabisa kwenye sheria zao. Aliyasema haya kwenye taadhima ya miaka 20 ya Itifaki ya Pili ya Khiyari ya Mapatano ya Kimataifa juu ya Haki za Kiraia na Kisiasa. Kwa mujibu wa Pillay, zile nchi zilizoridhia Itifaki hiyo, kwa upande wao, zinawajibika kutonyonga mtu anayehukumiwa adhabu ya kifo. Kadhalika, nchi hizi zinalazimika kuchukua hatua za kufuta kabisa adhabu ya kifo kwenye sheria zao na kuripoti utaratibu wanaochukua kutekeleza pendekezo hili. Juu ya hayo, nchi zilizoidhinisha Itifaki zinawajibika kutowarejesha watuhumiwa kwenye yale mataifa ambayo watakabiliwa na adhabu ya kifo.

Robert Serry, Mratibu Maalumu wa UM juu ya Mpango wa Amani kwa Mashariki ya Kati, kwenye taarifa aliowasilisha Ijumamosi, alisema alishtushwa na kuchukizwa sana na shambulio la msikitini lilioendelezwa mwisho wa wiki na walowezi wa KiIsraili, kwenye kijiji cha Yassuf, kiliopo katika eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan. Alisisitiza Serry kitendo cha "kunajisi mahali pa ibada kinakirihisha na huwakilisha tabia mbaya kabisa ya kiutu." Aliongeza kusema kwamba ni matumaini yake wenye mamlaka kwenye eneo husika, watawasaka na kuwashika wale walioendeleza tukio hilo pamoja na vitendo vyengine vya vurugu, na baadaye kuwafikisha mahakamani.