Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya Kimataifa ya Kuondoshwa Utumwa kuhishmiwa na UM

Siku ya Kimataifa ya Kuondoshwa Utumwa kuhishmiwa na UM

Tarehe ya leo, Disemba 02 (2009) huhishimiwa na UM kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Uondoshaji wa Utumwa.

Kwenye risala ya kuiadhimisha siku hii, KM alikumbusha kwamba kwenye hekaheka na harakati za walimwengu kung'ang'ania kusawazisha uhusiano wa kimataifa duniani, kumezuka mifumo mipya mengine ya utumwa, mathalan, ajira ya kulazimishwa, utoroshaji wa watu ambao hupelekwa kutumikia vibarua haramu nje ya makwao, na vile vile ujakazi haramu wa kijinsia, kama umalaya. Risala ya KM ilibainisha ya kuwa fungu kubwa la waathirika wa madhila haya huwa ni watu masikini na wale waliotengwa kijamii, kwa mfano, wale watu waliotoka kwenye jamii ya wachache na wahamaji. Alisema KM haitoshi kwa walimwengu kupambana na matatizo ya utumwa kwa kubuni sheria dhidi ya janga hili pekee, bali kunahitajika, vile vile, kujumuishwa kwenye vita hiyo, bidii ya pamoja ili kukomesha matatizo ya umaskini, hali ya kutojua kusoma na kuandika, ikichanganyika na uondoshaji wa tofauti na hitilafu za kijamii, pamoja na ukomeshaji wa ubaguzi wa kijinsia na ukomeshaji pia wa vile vitendo karaha vya kutumia mabavu dhidi ya wanawake na watoto.