Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Kabla ya kumaliza ziara ya siku moja mjini Washington D.C. mnamo siku ya Ijumanne, KM Ban Ki-moon alifanya mahojiano na waandishi habari, ambapo alitilia mkazo umuhimu wa kukamilisha mapatano yenye nguvu, kwenye mkutano ujao wa Copenhagen, itifaki ambayo itatumiwa kama ni msingi wa mkataba mpya wa kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa katika ulimwengu. KM alikiri, utekelezaji wa kadhia hiyo utahitajia gharama kadha wa kadha. Lakini vile vile alikumbusha ya kuwa gharama hizo hazitojumlisha fedha nyingi tukilinganisha na gharama zitakazorundikana kwa siku za baadaye, pindi walimwengu watashindwa kuchukua hatua zinazotakikana kudhibiti bora mabadiliko ya hali ya hewa kimataifa. Wabunge watatu wa Marekani walishiriki kwenye mahojiano hayo na waandishi habari, wakijumuisha Seneta John Kerry, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge juu ya Masuala ya Nchi za Kigeni, Seneta Richard Lugar na Seneta Joe Lieberman, kufuatia mkutano wa maseneta wengine na KM kuzingatia suala la mabadiliko ya hali ya hewa.

Shirika la Ulinzi Amani katika Cote d'Ivoire (UNOCI) limeripoti kuanza kutuma orodha ya muda ya wapiga kura katika maeneo yote ya nchi. Orodha hizo zilikabidhiwa Mjumbe Maalumu wa KM kwa Cote d'Ivoire, Choi Young-Jin Ijumanne na wawakilishi wa Kamisheni Huru ya Uchaguzi. Choi alisema hatua hii ni muhimu katika kuhitimisha mzozo uliolivaa taifa kwa miaka mingi, na alitumai jukumu liliosalia kuhusu upigaji kura - ikijumlisha uchapishaji na ugawaji wa vitambulisho vya kupigia kura - litakamilishwa haraka iwezekanavyo.

Marie Okabe, Naibu Msemaji wa KM, baada ya kuulizwa suala kwenye mahojiano ya adhuhuri na waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu, alithibitisha kwamba leo hii KM Ban Ki-moon alituma kwenye Baraza la Usalama, ripoti ya tume iliobuniwa kutafuta ukweli kuhusu mashambulio ya Tarafa ya Ghaza, tume iliyoongozwa na Jaji Richard Goldstone wa Afrika Kusini. Okabe alisema KM anaunga mkono kazi za tume na sasa hivi anasubiri uamuzi wa Barazala Usalama kuhusu hitimisho la ripoti.