Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya 2009 juu ya Kuangamizwa Vijibomu Vilivyotegwa Ardhini

Ripoti ya 2009 juu ya Kuangamizwa Vijibomu Vilivyotegwa Ardhini

Ripoti ya 2009 Inayosimamia Utekelezaji wa Kuangamiza Vijibomu Viliotegwa Ardhini, iliochapishwa Geneva hii leo, imeeleza kupatikana mafanikio kadha kwenye shughuli za kufyeka silaha hizo katika sehemu mbalimbali za dunia.

Ripoti iliwasilishwa rasmi kwenye Ofisi ya UM-Geneva na Taasisi ya Kampeni ya Kimataifa Kupiga Marufuku Mabomu Yaliotegwa Ardhini, na ilibainisha ya kuwa tangu Mkataba wa Kupiga Marufuku Mabomu Yaliotegwa Ardhini kuwa chombo cha sheria ya kimataifa miaka kumi iliopita, mafanikio ya kutia moyo yalishuhudiwa ulimwenguni katika kukomesha, na kuangamiza, silaha za vijibomu viliotegwa ardhini kuua wanadamu. Kwa mujibu wa ripoti, katika kipindi cha miaka kumi iliopita, biashara ya silaha hizi kimataifa, ikichanganyika na uzalishaji wa vijibomu na matumizi yake ilipungua kwa kima kikubwa kabisa. Ripoti ilieleza kilomita za mraba 3,200 zilifanikiwa kufyekwa mabomu yaliotegwa pamoja na viripuko, wakati idadi ya watu wanaojeruhiwa, kila mwaka, na silaha hizo, nayo pia iliteremka na ilijumlisha majeruhi 5,197 katika 2008. Lakini hata hivyo, ripoti ilikumbusha vizingiti kadha bado vimesalia, ambapo mataifa 70 yanaendelea kuathiriwa na silaha hizi, wakati misaada ya kuhudumia kihali majeruhi ni haba na hairidhishi.