Hatari ya nzige Mauritania imedhibitiwa kwa akali ya kutia moyo, imeripoti FAO

26 Oktoba 2009

Shirika la UM juu ya [Maendeleo ya] Chakula na Kilimo (FAO), limeripoti ya kuwa opereshini za kienyeji, za kudhibiti miripuko ya uvamizi wa nzige katika taifa la Mauritania, zimefanikiwa kuzuia wadudu hawa kutosambaa nchini au kuenea kwenye maeneo jirani ya mataifa ya kaskazini, na kuangamiza mazao na uwezo wa wakulima kupata riziki.

Taarifa ya FAO ilihadharisha pindi eneo hili la Afrika litabahatika kuepukana na mvua kali, inaashiria hatari ya nzige kutapakaa kwenye sehemu ya Afrika Kaskazini na Maghraibi, itakomeshwa kikamilifu itakapofika mwezi Disemba. Hivi sasa timu 17 zinazowakilisha Taasisi ya Taifa juu ya Nzige katika Mauritania, zinaendeleza uchunguzi na operesheni za kudhibiti uzalishaji wa nzige katika eneo la magharibi, ambapo mwanzo wa mwezi Oktoba kuligunduliwa maambukizo hatari ya nzige. Wafanyakazi wa Taasisi ya Mauritania walifanikiwa kuangamiza makundi 2,100 ya nzige tangu walipoanzisha operesheni zao katika tarehe 11 Septemba (2009). Mtaalamu anayeshugulikia udhibiti wa nzige katika FAO, Keith Cressman, alinakiliwa akieleza "hali ya nzige Mauritania hivi sasa, kwa ujumla, imeweza kudhibitiwa kama inavyostahiki", na FAO itaendelea kufuatilia, kwa ukaribu zaidi, hali hiyo, na kama kutazuka mabadiliko ya aina yoyote, FAO itaweza kuarifu mapema wadau wote husika, ikijumlisha nchi jirani na wahisani wa kimataifa, juu ya hatua za kuchukuliwa kidharura kujinusuru na miripiko haribiifu ya nzige kwenye eneo lao.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter