Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakutana kusailia uhusiano bora wa kulinda amani Afrika kati ya UM na UA

Baraza la Usalama lakutana kusailia uhusiano bora wa kulinda amani Afrika kati ya UM na UA

Asubuhi ya leo, kwenye ukumbi wa Baraza la Usalama, Manaibu KM wawili juu ya Masuala ya Ulinzi Amani - yaani Alain Le Roy, anayehusika na Operesheni za Ulinzi Amani, pamoja na Susana Malcorra, anayesimamia huduma za nje za mashirika ya ulinzi amani, waliwakilisha mapendekezo yao kuhusu hatua za kuimarisha, kwa vitendo, uwezo wa vikosi vya Umoja wa Afrika, kujenga na kudumisha amani kwenye maeneo yaliojivua kutoka vipindi vya fujo na vurugu, na vile vile walizingatia taratibu za kuimarisha uhusiano bora kati ya shughuli za UM na Umoja wa Afrika.

 Le Roy aliwakilisha ripoti ya KM iliotathminia mapendekezo ya Tume ya UM-UA iliobuniwa na Baraza la Usalama, ikijumlisha mapendekezo yanayoitaka UM kurekibisha huduma za mashirika yake yaliopo Addis Ababa, na kuipatia taasisi ya Umoja wa Afrika uwezo ziada wa kuendeleza zile shughuli muhimu zilizotambuliwa na wataalamu wa Tume. Le Roy, alisema yeye binafsi anaunga mkono rai ya Umoja wa Afrika kuimarisha majukumu ya kulinda amani wenyewe, pamoja na uhusiano wake na jumuiya za kiuchumi za kikanda. Lakini alisema angelipendelea kuona UA kuwa unafadhiliwa misaada maridhawa ya kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kama inavyopaswa. Vile vile alikumbusha kwamba katika miaka mitano iliopita ushirikiano wa mbinu za operesheni za ulinzi amani kati ya UM na UA, uliongezeka na kupanuliwa kwa kiwango kikubwa kabisa.